KITABUNI KUNA KITABU![Est 6:1 Vs 1 Kor 10:13]
“We will make electricity so cheap that only the rich will burn candles”
[Tutafanya upatikanaji wa umeme kuwa rahisi kiasi cha kuona matajiri pekee ndio wataotumia mishumaa].
Haya ni maneno ya Thomas Edson baada ya mawasilisho ya kwanza ya balbu mwanga ya umeme December 31, 1879[the first public presentation of his incandescent light bulb].
Ukifika pale Sweden siku ya tarehe 13 Disemba kila mwaka basi utakutana na asilimia kubwa ya Nchi imezungukwa na mishumaa mingi inayowaka kwani siku kama hii kila Mwaka pale Sweden wanaadhimisha siku ya Mtakatifu Lucia na inajulikana kama Lucia day. Siku hii kwao hutambulisha rasmi kuanza kwa kipindi cha Krismas, ambayo ni ishara ya Nuru katika jamii na taifa zima.
Na kama utasafiri mpaka Mexico majira haya ya Disemba basi usishangae utakapokutana na mishumaa imewashwa katika kona nyingi za nchi hii hasa wakati wa usiku kwa kipindi chote cha mwezi Disemba. Mexico majira haya husherehekea maisha ya waliokufa kwa kusimuliana michango chanya ya watu hao katika jamii katika kipindi cha uhai wao. Kwao ni moja ya wito kwa jamii kuishi maisha yenye kuacha alama nzuri ya kusaidia Taifa kwa vizazi hata vizazi.
Ukivuka mpaka na kusafiri mpaka Ugiriki(Greece) katika majira ya mwezi wa Februari mpaka Machi basi utastaajabu kuona mazingira yaliyopambwa na kupendeza kwa mishumaa yenye kutoa rangi mbalimbali. Inaitwa Easter Vigil. Wanasherehekea maadhimisho ya ufufuo wa Bwana wetu Kristo Yesu aliyeleta Tumaimi na kufanywa upya kwa waliomwamini.
Na kama wewe unawapenda sana Wabrazil na ukaamua kusafiri kwenda huko kipindi cha mwezi Juni, utakuwa umekwenda wakati mzuri sana ambapo utakuta familia zimekusanyika pamoja katika maeneo ya wazi huku mioto mikubwa(bonfires) ikiwaka nyakati za usiku na familia zikila, kunywa, kucheza pamoja na kuhubiriana Neno la Mungu pamoja kuomba kwa pamoja. Inaitwa FESTA JUNINA, sherehe ya kumkumbuka Yohana Mbatizaji kama moja ya Manabii wakubwa walioandaa mioyo ya watu kumpokea Kristo. Hivyo, kwao ni sherehe ya kuandaa mioyo yao kwa ajili ya kuendelea kupokea vyote vya Kristo.
Na kama wewe ni mfuatiliaji wa shughuli mbalimbali za sherehe za heshima hapa nyumbani kwetu Tanzania basi utakutana na mishumaa ikiwashwa katika maeneo hayo. Sehemu ambazo zinaonekana ni za heshima na kitajiri basi utakutana na mishumaa imewashwa.
Thomas Edson hakika alikuwa kama Nabii ambaye Neno alilozungumza hivi sasa linaishi. Umeme umekuwa na upatikanaji rahisi sana na hakika mishumaa imekuwa ikitumika katika shughuli zile za kitajiri tu kwa asilimia kubwa ulimwenguni kote.
Thomas Edson ni mwanasayansi aliyegundua mambo mengi sana. Senturi(phonograph), kamera ya picha ya mwendo(motion picture camera), bulb ya mwanga(light bulb).
The Wizard of the Menlo Park ndilo jina ambalo wasomi wa nyakati zake walimuita Thomas Edson hasa baada ya kuwasilisha kwa mafanikio bulb ya mwanga ya kwanza ya umeme. Walimuona kama mtu ambaye alifanya mambo ambayo ni ngumu kufikirika kwa mwanadamu wa kawaida. Japokuwa wengi walishafanya gunduzi za bulbu ya mwanga lakini mpaka wakati wake Thomas hakukuwa na mwanasayansi aliyefanikiwa kugundua bulbu ya mwanga ya umeme. Jambo lililoonekana gumu kwa wengi likafanywa na bwana Thomas Edson.
Wasilolijua wengi ni kwamba kabla Thomas Edson hajawa mgunduzi wa kisayansi aliyejulikana kwa watu, Thomas alianza kuwa mgunduzi nyumbani.
Kipindi pekee ambacho Thomas alikwenda katika masomo ya shule hizi za mitaala ya kidunia(formal education) ni kipindi alipokuwa na miaka 17. Kipindi ambacho alikwenda kusomea mambo yaliyohusu Kemia(Chemistry) na electricity(umeme).
Jambo pekee lilifanya wazazi wake wampeleke katika shule hiyo ni ili kuendeleza ugunduzi wake wa kisayansi ambao aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka mitano(5). Wazazi walifahamu kuwa dunia ingeweza kumkataa kama asingelikuwa na vyeti vya elimu ya duniani.
Thomas Edson alifundishwa kusoma na kuandika nyumbani, na mama yake mzazi ndiye aliyekuwa mwalimu wake wa kwanza. Baadaye baada ya wazazi wake kuona kuona hali ya mtoto wao kupenda sayansi na teknolojia waliamua kuigeuza karakana yao ya nyumbani kuwa chumba cha maabara kwa ajili ya majaribio mbalimbali ya ugunduzi wa kisayansi.
Walimwezesha kwa kila kitu alichohitaji kwa kazi zake. Wakati fulani familia ya Thomas Edson ilipitia ukata mkubwa jambo lililomfanya Thomas akiwa na umri wa miaka 11 kuanza biashara ya kuuza magazeti ambapo kufikia umri wa miaka 13 aliweza kutengeneza faida ya dola 50 kwa wiki.
Akiwa na umri wa miaka 15, Thomas Edson alimuokoa mtoto wa miaka mitatu Jimmie MacKenzie kutoka katika kutaka kugongwa na gari moshi(treni). Jambo hili lilimfanya baba wa mtoto huyo kumchukua Thomas na kuanza kumfundisha kuwa mwendeshaji wa telegraph(telegraph operator).
Thomas alifanikiwa kuwa mwendeshaji wa telegraph na miezi michache baadaye akaajiliwa katika kampuni moja ya telegraph hata hivyo hakuweza kudumu kwa muda mrefu kutokana na uharibifu aliofanya katika ofisi yake usiku mmoja alipojisahau na kuanza kufanya majaribio yake ya kisayansi ofisini na kusababisha kuungua kwa baadhi ya nyaraka za ofisi kwa kemikali zilizomwagika.
Thomas alikwenda kuajira baadaye katika kituo kimoja cha uwakala wa treni ambapo napo ndani ya mwaka mmoja aliamua kuacha kazi baada ya kusababisha treni mbili za mafunzo kugongana wakati yeye alipokuwa akisoma vitabu kwa ajili ya kuendelea kunoa akili yake.
Mazingira yote haya yalimfanya Thomas Edson kugundua uwezo mkubwa wa kufanya biashara aliokuwa nao, mbali na uwezo wa kugundua mambo ya kisayansi.
Na hapo akaamua rasmi kufungua maabara yake kwa kushirikiana na akina Henry Ford ili aweze kuendeleza kazi zake za uvumbuzi na ugunduzi.
Tangu hapo, Thomas amekuwa akifanikiwa siku hata siku na hatimaye mwaka 1879 kwa mara ya kwanza aliwasilisha katika bodi ya wanasayansi balbu ya mwanga ya umeme ya kwanza kufanikiwa kuwaka ambayo ilikuwa na uwezo wa kutumika kwa zaidi ya masaa elfu kumi na mbili(12000).
Ugunduzi huo ndio uliofanya aongee kwa ujasiri maneno niliyoanza nayo katika makala hii, kwani ni ugunduzi uliochochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda duniani kote.
Thomas Edson, Mwanasayansi aliyezaliwa nyumbani, akakuzwa nyumbani na kufanikiwa sana kutokana na elimu ya nyumbani.
Mwana wa Mungu, nikuulize swali…
Nyumbani kwako kuna wakina nani?
Usiache kutuandikia maoni yako ili nasi tuzidi kuviandika vitabu vingi hapa Kitabuni.
Na;
Mwandaaji na Mwandishi,
Mchungaji wa Kristo Erney Mbala,
Huduma Ya Kimataifa Ya Kimataifa Ya Pete Ya Muhuri Haggai 2:23,
Dar es salaam.
WhatsApp: 0682632323
Email: chotimbala@gmail.com